KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimemtaka Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, kuwaomba radhi Watanzania kutokana na kutoa kauli ya kukatisha tamaa.
Simbachawene, juzi alitoa kauli ya serikali ya kupandisha bei ya
umeme kama Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), lilivyoomba hivi
karibuni kutaka kuongeza gharama za nishati hiyo kwa asilimia 68.
Alisema ni ukweli usiopingika kuwa hata TANESCO ikiongeza gharama za
umeme hadi kufikia sh 800 kwa uniti bado bei hiyo itaendelea kuwa nafuu
ukilinganisha na gharama za kununua mafuta ya taa.
Simbachawene alitoa tahadhari kwamba endapo kuna mwananchi yeyote
atakayeona gharama za umeme ni kubwa ni vema akaamua kuwasha kibatari
au akae gizani.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano jana, Mkurugenzi wa Kituo
hicho, Dk. Helen Kijo-Bisimba, alisema kuwa kauli hiyo inaweza
kusababisha vurugu kutokana na suala la umeme kumgusa kila Mtanzania.
Alisema kuwa hivi sasa viongozi wamekuwa wakitoa kauli za kuudhi ambazo ni hatari kwa ustawi wa taifa.
“Tunakumbuka kauli za kuudhi zinavyozidi kushamiri wakti ule
aliyekuwa Waziri wa Fedha Basili Mramba alipowaambia Watanzania
wajifunge mikanda kubana matumizi hata ikibidi kula majani watakula,
lakini ndege ya rais lazima inunuliwe; akaja Waziri wa Ujenzi John
Magufuli aliyewaambia wakazi wa Kigamboni kuwa kama hawawezi kulipa
ongezeko la nauli mpya basi wajifunze kupiga mbizi, ili kuvuka kwa
kuogelea, wanaporudi vijijini au wazunguke kupitia Kongowe sasa hii ya
vibatari!”alisema.
Alisema kuwa ni muhimu viongozi wakahakikisha wanatoa kauli zilizo na hekima ili kuepusha migogoro.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa baada ya serikali kupandisha gharama hizo, muathirika mkubwa ni mwananchi wa chini.
Alisema kuwa wamiliki wa viwanda wanachoangalia ni faida hivyo
kupanda kwa bei ya umeme kutasababisha gharama za bidhaa kuzidi kuwa
juu zaidi.
“Nchi za wenzetu hakuna jambo linaloweza kufanywa bila kushirikisha
wananchi lakini hapa kwetu wanaamua tu na mbaya zaidi wanakuja na kauli
za kuudhi na kukatisha tamaa kwa kuwa Watanzania ni wapole,” alisema.
Dk. Bisimba alisema kuwa ni lazima wafahamu kuwa upole wa Watanzania
utafikia kikomo na hiyo inaweza kusababisha hatari kwa taifa.
Wiki hii wadau mbalimbali wa umeme likiwamo Shirikisho la Wenye
Viwanda Tanzania (CTI) na Baraza la Ushauri la Watumiaji Huduma za
Nishati na Maji (EWURA CCC), walipinga maombi ya Shirika la Umeme
Tanzania (TANESCO) ya kuongeza gharama za umeme kwa asilimia 67.8.
Walisema ongezeko hilo ambalo limelenga zaidi viwanda vikubwa na vya
kati litasababisha kupanda kwa bei za bidhaa za viwandani.
Mjumbe wa Bodi ya CTI, Samuel Nyantahe, alisema kabla TANESCO
haijapandisha gharama hizo ingekusanya madeni yote na kuziba mianya ya
wizi wa umeme.
Naye Mjumbe wa CCC Thomas Mnunguli, alisema ongezeko hilo ni kubwa na
linakosa uhalali hivyo TANESCO ijitathmini na kujipanga upya na ilenge
kutoa huduma bora na nafuu.
-Tanzania Daima
-Tanzania Daima