WAKATI Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikimwandikia Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe barua ya kumtaka ajieleze dhidi ya tuhuma zinazomkabili, yeye ameamua kukimbilia polisi akimshitaki mmoja wa viongozi wenzake.
Habari za kuaminika zimedai kuwa Zitto ambaye hivi karibuni alivuliwa
cheo chake cha unaibu katibu mkuu wa CHADEMA, inadaiwa amefungua
mashitaka polisi akimtuhumu Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Dar es Salaam,
Henry Kileo kwa madai ya kusambaza waraka katika mitandao ya kijamii.
Akithibitisha tukio hilo, wakili wa Kileo, Peter Kibatara, alisema
kuwa mteja wake amemriwa kufika makao makuu ya Jeshi la Polisi leo
Jumatano saa nane mchana na kuonana na mmoja wa maofisa wa juu wa jeshi
hilo, aliyetajwa kwa jina moja tu la Mbutta, kufuatia mashitaka
yaliyofunguliwa na Zitto dhidi yake.
Akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wetu, Kileo
alikiri kuitwa polisi, ingawa alidai hajui ni waraka gani anaotuhumiwa
kuusambaza unaomchafua Zitto.
“Kwa kweli sijui hata mimi ni waraka gani, ingawa hivi karibuni
kulikuwa na waraka wa siri uliodaiwa kutoka CHADEMA, na ambao ulijaa
tuhuma za usaliti. Lakini huo tuliishaukana siku nyingi. Labda kuna
mwingine,” alisema Kileo.
Zitto kutwa nzima ya jana hakuweza kupatikana kwa njia ya simu
kufafanua mashitaka aliyofungua polisi. Simu zake zote za kiganjani
zilikuwa zimezimwa.
-Tanzania daima
-Tanzania daima