WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe na Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, wameunda kamati ndogo ya wataalamu kwa ajili ya kutatua changamoto zilizopo magerezani.
Wakizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanya ziara katika magereza yaliyopo katika jiji la Dar es Salaam, mawaziri hao wakifuatana na makatibu wakuu wao, walisema wameshuhudia shangamoto kadhaa ambazo wameamua kuziundia kamati kwa lengo la kuzitatua.
“Leo tumezunguka katika magereza na tumeshuhudia changamoto kadhaa ambazo tunaunda kamati ndogo ya wataalamu, kutatua changamoto hizo na Januari tutarudi tena huku tukiwa na baadhi ya majibu ya baadhi ya changamoto hizo na kuwaeleza wapi tumefikia katika kutatua changamoto nyingine,” amesema Dk Mwakyembe.
Dk Mwakyembe alisema ana matumaini makubwa kwamba watafika mbali katika matarajio ambayo Rais John Magufuli anatarajia kuifikisha nchi, ambapo alitaja changamoto walizozishuhudia kuwa ni pamoja na msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani, uhaba na uchakavu wa nyumba za askari pamoja na ubovu wa miundombinu iliyopo magerezani na vitendea kazi.
“Serikali hii ya Awamu ya Tano kama ambavyo mmeona, imeanza kwa kasi ya kuwaletea matumaini makubwa wananchi, matumaini ambayo yanahitaji wizara zote kutengeneza mazingira wezeshi kuleta mabadiliko makubwa,” alisema Dk Mwakyembe.
Alisema moja ya Wizara muhimu zinazotegemewa kutengeneza mazingira wezeshi ili kupiga hatua ni wizara zao kwa sababu zina vyombo vinavyotoa huduma za haki kwa wananchi katika kukamata, kufungua mashitaka, kuhukumu na kuhifadhi watu gerezani.
Kutokana na mambo hayo, ndiyo maana waliamua kufanya ziara ya pamoja kutembelea mazingira ya magereza ya Segerea, Keko na Ukonga, kujifunza changamoto zilizopo katika magereza hayo ili waweze kuunganisha nguvu kutatua changamoto hizo.
Alisema katika msongamano magerezani, wamejifunza magereza yamekuwa yakibeba zaidi ya mara mbili ya uwezo wa magereza hayo na hiyo inatokana na ucheleweshaji wa kesi, unaofanyika katika vyombo ambavyo viko chini ya wizara hizo