Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema na kuungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa amesema anashangaa kuona anaambiwa mleta vurugu wakati dunia inamkubali kuwa ni mlinzi wa amani.
Kauli ya Lowassa imekuja ikiwa ni siku moja baada ya taasisi za kidini 1,200 duniani kupitisha jina lake kwa ajili ya kumpatia Tuzo ya Amani.
“Nimepokea kwa unyenyekevu na furaha tuzo ya amani duniani ninayotarajiwa kupewa na taasisi za kidini 1200 duniani,” alisema Lowassa akinukuliwa na msemaji wake, Aboubakar Liongo.
Lowassa alisema tuzo hiyo ni kithibitisho cha uongo wa CCM na Serikali yake kuwa wapinzani ni watu wa vurugu.
Taasisi hizo katika kikao chake huko Bukavu DR Congo, zilitangaza kumpa tuzo hiyo Edward Lowassa kutokana na utulivu aliyouonyesha kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu Kwa jamii, Mchungaji William Mwamalanga ilisema kiasi wajumbe 1,400 wa mkutano huo kutoka kote duniani walikubaliana kumpa tuzo hiyo Lowassa kati ya wanasiasa 1,000 waliyoshindanishwa ili kumpata kiongozi bora wa Amani mwaka 2015, ambaye anajali na kuangalia maslahi ya jamii badala ya madaraka.
Alisema yeye ni muungwana na ana hofu ya Mungu na hata siku moja hatoweka mbele maslahi binafsi, na ndiyo maana aliwatuliza wananchi waliyokuwa wakimtaka kutoa tamko baada ya matokeo kutangazwa.
“Siko tayari kuingia Ikulu huku mikono yangu ikibubujika damu. Nashukuru taasisi hizo za kidini duniani, zimeliona hilo,” alisisitiza Lowassa