JUMBA linalodaiwa kutumika kuendesha shughuli za ukahaba limebainika kuwapo katika eneo la Buguruni, jijini Dar es Salaam.
Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwapo kwa jumba ambalo linatumika kama
nyumba ya kulala wageni, ambako idadi kubwa ya makahaba hujazana na
kuendesha biashara ya kuuza miili yao bila wasiwasi.
Wasichana wanaofanya biashara hizo hutoza kiasi cha sh 5,000 kama huduma ya ngono na chumba kwa matumizi ya muda mfupi.
Biashara hiyo ambayo imeleta usumbufu mkubwa kwa wakazi wengi
wanaopakana na nyumba hiyo, imekuwa ikifanikiwa kutokana na kuwapo kwa
baadhi ya askari polisi wanaodaiwa kuwalinda wasichana hao pamoja na
mmiliki wa nyumba hiyo.
Nyumba hiyo inavyo vyumba vingi vinavyotozwa kiasi sha sh 1,200 kwa
chumba pamoja na kondomu. Kadhalika wasichana wenye umri wa miaka 15, ni
miongoni mwa wanaofanya biashara hiyo.
Mjumbe wa serikali ya mtaa wa eneo hilo, Amiri Banza, alikiri kuwapo kwa
biashara hiyo, ingawa alisema wamejaribu sana kuzuia hali hiyo bila
mafanikio:
“Tumechoka na hii kadhia, tumeripoti kwa viongozi wa Kata hadi polisi
lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa. Kama wakija polisi
wanawakamata, halafu wanawaachia,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi wa Ilala, Marietha Minangi
alipoulizwa juu ya kuwapo kwa jumba hilo alisema hajui chochote.:“Mimi
sijapata taarifa hizo na ndiyo kwanza ninakusikia wewe,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu polisi kufika kwenye jumba hilo na kuchukua rushwa na
kuondoka alisema: “Sina ushahidi, kama wapo polisi wanafanya hivyo ni
kosa,” alisema Minangi na kuongeza kuwa polisi wanafanya doria maeneo
hayo na mara kadhaa wamewakamata watu wanaojihusisha na vitendo hivyo na
kuwafikisha mahakamani