Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amesema kuwa ataisimamia sheria namba 30 ya mwaka 1973 ya usalama barabarani iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2001 inayohusu kiwango cha mwisho cha uzito wa magari pasipo kumwogopa mtu yeyote kwa kuyatoza magari yote yatakayozidisha uzito.
Kadhalika, ametoa wito kwa wakandarasi nchini kujenga barabara zenye
viwango huku akiwataka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kusimamia
sheria kwa yeyote atakayekiuka makubaliano ya mkataba.
Aliyasema hayo jana wakati wa uwekaji saini wa mradi wa ujenzi wa
barabara za Dodoma-Babati na Tunduru, Mangaka- Mtambaswala kati ya
Tanzania na Benki ya Maendeo Afrika (ADB) na Shirika la Kimataifa la
Maendeleo la Japan (Jica) wenye thamani ya Sh. bilioni 538.8. Dk.
Magufuli alisema barabara nyingi za nchini zinaharibika kutokana na
magari ya mizigo kuzidisha uzito.
Alisema serikali isiposimamia sheria hiyo barabara zitakuwa zinaharibika
kila mara, na mwishowe mikopo hiyo italipwa na Watanzania maskini
katika kodi zao huku barabara hizo zikiwa mbovu.
“Hizi fedha tumekopeshwa sisi na watakaolipa ni Watanzania, hivyo
wakandarasi mnatakiwa kujenga barabara zenye viwango na nyie Tanroads
mhakikishe mnayabana magari yaliyozidisha uzito,” alisema Dk. Magufuli.
Aliongeza kuwa serikali haitakuwa tayari kurudia rudia kujenga barabara
moja mara mbili kutokana na uzembe wa watu wachache wanaoharibu
barabara, na kuwataka wakandarasi nchini kujenga barabara zenye ubora.
Dk. Magufuli alisema sehemu nyingine magari ya mizigo yana viwango vya
uzito akitolea mfano Marekani kuwa ni tani 36.2, Uingereza tani 40,
Ujerumani tani 40. Ufarasa tani 40, Urusi tani 38, lakini kwa Tanzania
ni tani 56 ambacho ni kiwango kikubwa.
“Na nitaendelea kusema ukweli pasipo kumwogopa mtu hadi naenda kaburini,
gari lolote litakalozidisha mzigo nitalitoza faini kwa mujibu wa
sheria, tunataka barabara zetu zidumu kwa miaka mia moja,” alisema Dk.
Magufuli.
Dk. Magufuli alisisitiza kuwa ikiwa serikali itaamua kuyaachia magari ya
mizigo kuzidisha kiwango cha uzito, barabara zitaendelea kuharibika
kila siku.
Waziri Magufuli aliwataka wahandisi wa mikoani kusimamia miradi hiyo ya
barabara na kueleza kuwa miradi hiyo ikifeli na wahandisi wao watakuwa
wamefeli.
Dk. Magufuli ametoa kauli hiyo wakati mgogoro baina ya serikali na wasafirishaji nchini kabla haujapata ufumbuzi.
Wasafirishaji hao Chama cha Wamiliki wa Malori (Tatoa) na Chama cha
Wamilikiwa Mabasi (Taboa) Oktoba 8 na 9, mwaka huu waligoma wakipinga
kufutiwa msahama wa kutozwa faini asilimia tano kwa kuzidisha uzito.
Mgomo huo ulifuatia tangazo la waziri magufuli Oktoba Mosi, mwaka huu kufuta msamaha huo na kurejesha sheria ya mwaka 1973.
Baada ya mgomo huo uliotikisa nchi, Oktoba 10, Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda, aliingilia kati na kusitisha tangazo la Dk. Magufuli huku akitoa
mwezi mmoja kwa serikali kukutana na wadau wa usafirishaji kupata
mwafaka.
Hata hivyo, hadi kumalizika kwa muda huo mwafaka haujapatikana huku
serikali ikisema timu hiyo imeanza kazi wakati wadau wa usafirishaji
wakisema hawajashirikishwa.
Jana NIPASHE lilimtafuta Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu, ambaye
alisema kwa sasa hawatozwi tozo yoyote isipokuwa wanaiomba serikali
kuyaruhusu mabasi kutoingia kwenye mizani kama nchi zingine za Afrika
Mashariki zinavyofanya.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Florence Turuka, alisema timu ya
kusaka mwafaka wa mgogoro huo na wadau wa usafirishaji inaendelea na
vikao, na kueleza kuwa kikao cha mwisho kilifanyika Novemba 29, mwaka
huu.
Aliongeza kuwa wiki hii timu hiyo iliyojumuisha wanasheria kutoka
Wizara ya Uchukuzi, Ujenzi, Wizara ya Viwanda na Biashara, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Taboa na Tatoa
wanatarajia kukaa tena.
Alisema timu hiyo inatarajia kumaliza vikao vyake Desemba 10, mwaka huu,
na mpaka sasa wameshapitia hadidu za rejea mbalimbali zilizowasilishwa
na wajumbe wa timu hiyo.
ATHARI ZA MGOMO
Mgomo wa wasafirishaji ulisababisha Bandari ya Dar es Salaam kuelemewa mizigo.
Takribani tani 23,165 za mbolea ambazo zilikuwa zimeshushwa bandarini hapo zilikwama kutokana na kutokuwapo kwa malori.
Kadhalika, takribani meli tisa za mizigo zilikwama kushusha na kupakia mizigo bandarini.
Vile vile, uwezo wa kushusha makontena katika bandari hiyo ulishuka kutoka makontena 800 kwa siku hadi 300
-NIPASHE-