Kitendo alichofanyiwa mwanamuziki wa Bendi
ya FM Academia ya jijini Dar anayejulikana kwa jina moja la Flora
alfajiri ya kuamkia Desemba 8, mwaka huu ni kibaya katika jamii ya
Kitanzania.
Flora akiwa amepata kinywaji ili kuchangamsha mwili wake alijikuta
akipigwa na vijana wawili wanaofanya kazi ya kuendesha Bajaj akiwa
amewakodi kwa ajili ya kurudi nyumbani kwake.
Tukio hilo lilitokea maeneo ya Mwananyamala jirani na MK Pub jijini
jirani kabisa na ofisi ya Msanii Tuesday Kihangala ‘Mr Chuz’ limeacha
simanzi kubwa kwa wakazi wa eneo hilo.
Kwa mujibu wa shuhuda wetu inadaiwa kuwa, Flora alipigwa na vijana
hao na kuporwa vitu vyake vya thamani ikiwemo simu pamoja na pochi
lililokuwa na kiasi cha fedha ambavyo vyote bado havijajulikana thamani
yake.
Mbali na kumpiga, vijana hao waliokuwa wakisaidiana
kufanya kazi katika Bajaji hiyo wanadaiwa kumvua nguo mwanamuziki huyo
ambaye aliwahi kutunga na kuimba kibao cha Sintasahau huku akishiriki
kuimba vibao vingine vya FM Academia kama vile Dunia Kigeugeu, Shida na
Heshima kwa Wanawake.
“Tulikuwa tumekaa naye hapa tukila chips (MK) baada ya kumaliza kula
Flora alionekana akikodi Bajaj ili kurudi nyumbani kwake, baada ya muda
tukawaona watu wakikimbilia kule kwenye ofisi ya Chuz, tulipoenda
tukamkuta Flora akipewa msaada na mlinzi na mwanamuziki mwingine
kutokana na unyama aliofanyiwa,” alisema shuhuda huyo.
Naye mlinzi aliyekutwa eneo la tukio alipoulizwa kuhusina jinsi
kitendo hicho kilivyotokea, alisema kuwa aliiona Bajaj ikisimama eneo
hilo na watu wanne wakashuka akiwemo Flora na baada ya muda kidogo
alimuona mtu akijikokota alipomsogelea ndipo alipomuona mwanamuziki
huyo akiwa amevuliwa nguo.
“Wamemfanyia unyama sana wale vijana, sijui nini kingetokea kama
ningegundua kabla hawajatenda unyama wao,” alisema mlinzi huyo
aliyekataa kutajwa jina lake gazetini.
Flora aliondolewa eneo hilo baada ya kupewa msaada wa nguo na mmoja wa majirani wa eneo hilo ili ajisitiri.
Baada ya tukio hilo, mwandishi wetu alimpigia simu Kiongozi wa FM
Academia, Nyoshi El Sadaat lakini hakuweza kupokea ndipo akahamia kwa
mwanamuziki wa bendi hiyo, Patcho Mwamba na kumuuliza kama Flora bado
yuko FM Academia.
Patcho alikiri uwepo wa Flora katika bendi yao lakini alisema kwamba
siku hizi mbilI hajaonekana na alisikitika alipopewa kisanga hicho
kilichomkuta.
“Ni kweli tunaye Flora lakini siku hizi mbili hakuwepo kazini dah!
Wamemfanyia unyama sana, madereva wengine wa Bajaj si watu wazuri,“
alisema Patcho.
Mpaka sasa haijajulikana kama Flora alitoa taarifa za tukio hilo polisi au la, jitihada za kumtafuta zinaendelea.
--GPL--