KATIBU
Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ametoa neno
endapo Rais John Magufuli atamhitaji kuendelea na wadhifa huo, huku
akibainisha kuwa amekutana na changamoto nyingi katika nafasi hiyo kiasi
kwamba wakati mwingine alikata tamaa.
Mwanasiasa huyo maarufu ndani ya CCM na nchini, anatarajiwa kuhitimisha uongozi wake wiki hii wakati Mwenyekiti mpya wa CCM Taifa, Rais John Magufuli atakapokabidhiwa uenyekiti huo na kuunda Sekretarieti yake mpya ambayo haijulikani kama itaongozwa tena na Kanali huyo wa zamani wa Jeshi.
Akizungumza
jana na waandishi wa habari baada ya kukagua Ukumbi wa Mkutano Maalumu
wa CCM utakaofanyika keshokutwa Jumamosi, Kinana ambaye amekuwa katika
nafasi hiyo kwa miaka mitatu na nusu, alisema aliombwa katika nafasi
hiyo baada ya kuwa aliamua kustaafu, lakini akakumbana na changamoto
mbalimbali.
CCM kuwa mbali na wananchi
Alisema kuna wakati aliona kama vile chama kiliacha kwenda kwa wananchi na kwamba hakikuwa karibu sana nao.
“Ninyi
ni mashahidi, ikabidi kubuni utaratibu mzuri wa kwenda kwa wananchi ili
chama kiwe karibu na wananchi, kiwasikilize na kuwa sauti ya wananchi
kifuatilie matatizo yao kisimamie utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi,”
alisema Kinana na kuongeza kuwa katika kufanya hivyo amekuwa
akiwasiliana na Rais na Waziri Mkuu kwa ajili ya matatizo kutatuliwa.
“Changamoto
ya pili ya kuimarisha umoja na mshikamano ndani ya chama, hapo nyuma
kulikuwa na misukosuko kidogo ya umoja na mshikamano, kushutumiana na
kulaumiana,” alisema na kuongeza kuwa kazi nyingine aliyofanya ni
kuimarisha umoja ndani ya chama, kushirikiana na viongozi wenzake
kuhakikisha chama kinajitahidi kwa kadri ya uwezo wake kurejea katika
misingi yake ya awali katika maeneo ya uadilifu, uwajibikaji na utendaji
kazi kwa ufanisi.
Azuiwa ziarani
Kinana
alisema amekwenda wilaya zote, majimbo, mikoa na nusu ya kata za nchi
na amesafiri zaidi ya kilometa 192,000, kufanya mikutano zaidi ya 3,700
ya aina mbalimbali ya ndani na nje na haikuwa kazi rahisi
“Changamoto
nilizokutana nazo ambazo lazima nikiri ni pale nilipotaka wakati
mwingine kufanya ziara kwenye maeneo fulani fulani niliambiwa ni
hatarishi siwezi kwenda kwa hiyo ilibidi nibishane na viongozi na
watendaji wakuu wa serikali…nikasema hapana nimeamua kwenda lazima
niende,” alisema Kinana.
Katibu
huyo akitoa mfano alisema kuna wakati aliamua kutoka kwa boti kutoka
Nyamisati wilayani Rufiji kwenda Mafia, viongozi wa Mkoa wa Pwani
walifikiri si njia salama ya kusafiri na kumpelekea ujumbe asisafiri kwa
boti, bali asafiri kwa ndege, lakini alisema hapana ataondoka kwa boti.
“Walichofanya
wakakaa kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na wakaniandikia
barua rasmi kwamba tunakushauri usisafiri kwa boti safiri kwa ndege kwa
maana nyingine walikuwa wanajivua lawama kwa yatakayotokea, lakini vile
vile kunitisha kidogo kwamba si salama zaidi nikawasisitiza hapana,” alieleza Kinana.
Ashitakiwa kwa JK
“Baadaye
Rais mstaafu Kikwete alikuwa Msoga, viongozi wa Mkoa wa Pwani wakaenda
kumwambia tumezungumza na Katibu Mkuu wako naona hasikii tumemuandikia
barua ya kumuomba asisafiri na boti hasikii, Rais akaandika meseji ndefu
sana…nikamjibu rais nakuheshimu mamlaka yako ni makubwa si vizuri
nikakukatalia, lakini niruhusu nikukatalie kwa sababu hata wananchi
wanaosafiri kwenye boti hii wanahatarisha maisha yao, ni vizuri na mimi
nikahatarisha maisha yangu hata kidogo… akaniambia nimekuelewa endelea,” alibainisha.
Alisema
zipo changamoto nyingi sana nyingine, kwa mfano Mbambabay kwenda Kyela,
mkuu wa mkoa akamuambia boti haifai kusafiri akasema mara haiwezi
kusafiri imeharibika.
“Nikazungumza
na Mwakyembe akapeleka mafundi wakatengeneza, safari haikuwa rahisi,
lakini changamoto zilikuwa nyingi sana, kwingine Lupingu kule ni gari
moja tu ndio inayoshuka chini hakuna kupishana magari nikaambiwa
nisiende nikasema nina kwenda,” alisema na kuongeza kuwa kulikuwa na ubishi mwingi wakati mwingine alionekana mtu mmoja kidogo ambaye hasikilizi ushauri sana.
Pia
nyingine zinazotokana na changamoto za wananchi kutolipwa mazao yao kwa
wakati, mbolea kutofika kwa wakati, halmashauri kutopata fedha za
maendeleo kwa wakati, watumishi wa umma wanaohamishwa kwenda vijijini
hawaendi vijijini kwenda kuwahudumia wananchi, tatizo kubwa la migogoro
kati ya wakulima na wafugaji kati ya wananchi na hifadhi za taifa.
“Ndio
maana mnaniona siku hizi nimenyamaza kwa sababu yale yote niliyokuwa
nikiyaombea yanafanyika, umangimeza haupo watu wachape kazi wawahudumie
wananchi, uadilifu unapigwa vita, rushwa inapigwa vita, uwajibikaji na
uadilifu unahimizwa, utendaji kazi unatakiwa na hayo yasipofanyika mtu
anaondolewa mara moja,” alifafanua Kinana ambaye kuanzia mwaka 2014
hadi mwanzoni mwa mwaka jana alitembea kote nchini akikisafisha chama
chake na kuibana serikali.
Kurejea kwake CCM
“Yalitokea
mazingira ambayo niliombwa na viongozi wastaafu na viongozi wa chama
kuniomba niwe mtendaji mkuu wa chama chetu. Si nafasi ambayo niliipenda,
bali niliitwa na nikakalishwa wakanisihi na mimi nikakubali sababu ni
wito na kwa kuwa ni watu ninaowaheshimu na wana dhamana kubwa kwenye
nchi yetu, nikakubali kufanya kazi hiyo,” alisema Kinana akizungumzia jinsi alivyoteuliwa kushika nafasi hiyo.
Alisema
amekuwepo katika uongozi ndani ya chama kwa muda mrefu (miaka 25) ndani
ya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa, na alihisi ni wakati muafaka
wa kung’atuka.
“Mwanasiasa
mzuri ni yule anayejua wakati wa kuingia na wakati wa kutoka. Ni wakati
mzuri wa kung’atuka kuachia waingie wenye umri wa kati na umri wa
vijana kuachia waongoze chama na kuwaamini,” alieleza.
Alisema
moja ya mambo ambayo walikubaliana wakati ule akajitahidi kukiimarisha
chama, kusimamia na kumsaidia mwenyekiti kusimamia mchakato wa kuwapata
wagombea kwenye nafasi zote za Urais, Ubunge na Udiwani. Pia alijitahidi
kuendesha shughuli za kampeni na uchaguzi na utakamalizika.
“Uchaguzi
umekwisha niruhusiwe kupumzika, na wote waliafiki na kukubali sasa muda
umefika kwa hiyo nimewakumbusha yale tuliyokubaliana muda wake umefika
sasa wengine wakaniuliza hivi ndivyo tulivyokubaliana nikawaambia wazee
hamjawa wazee kiasi cha kusahau ndio haya tuliyokubaliana,” alieleza.
Akiombwa na JPM
Alipoulizwa kama akiombwa na Rais Magufuli aendelee kwa Katibu Mkuu, Kinana alisema, “Niseme
hajasema, hatujazungumza hilo, likitokea tutaangalia, tutakaa naye
kikao kama akiniomba, tutakuwa na kikao na mazungumzo muda utakapofika
kama nilivyokuwa na mazungumzo na kikao kama kwa wale walioniomba mwaka
2012.”
Waliokisaliti chama
Akizungumzia
walioisaliti CCM katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana, mtendaji huyo wa CCM
alisema msaliti yeyote adhabu yake ni mbaya sana, hata kwenye chama cha
siasa.
“Kwenye
CCM wapo watu walioyumba, kulikuwa na wimbi kubwa mwaka jana, watu
waliyumba hivi kidogo wakakaa mguu upande huku hawapo na kule hawapo,
wako ambao sio tu waliyumba, bali walikiuka maadili na hawakushiriki
kwenye shughuli za kampeni,” alisema.
Pia
alisema wapo ambao hawakushiriki, hawakusaidia na wakasaidia upinzani
na kila mtu atakuwa na adhabu yake kulingana na makosa yake.
“Kama
mmekuwa mkifuatilia kuna waliochukuliwa hatua ngazi za wilaya na mikoa.
Kwa mfano, Shinyanga 123 walichukuliwa hatua. Wapo wanaotakiwa
kuchukuliwa hatua kwenye ngazi za juu, sasa jambo moja mtu yeyote kabla
ya kuchukuliwa hatua lazima aelezwe mashtaka yake, apewe fursa ya
kusikilizwa, kwa hiyo hawa wote watasomewa mashtaka, watasikiliza na
kupewa adhabu kwa kadri itakavyostahili, lakini hatua zitachukuliwa mara
baada ya Mkutano Mkuu kumalizika,” alieleza.