Kwa mujibu wa chanzo makini cha gazeti hili, wanaume wengi wamekuwa wakimendea kufunga ndoa na Lulu lakini wakashindwa njia za kumpata.
Ilidaiwa kuwa kikwazo kikubwa wanachokutana nacho ni namna ya kumfikia na kigezo cha dini kwa sababu Lulu hataki kuolewa na muislam kwani hayupo tayari kubadili dini.
Akizungumza na Amani katika mahojiano maalum, mapema wiki hii, mama wa Lulu, Lucresia Karugila alisema kwa upande wake yupo tayari kupokea mahari yoyote ilimradi mwanaye awe ameridhiana na mwanaume husika.
“Unajua Lulu ameshakua, mambo ya kumwingilia mtoto kwenye vitu binafsi ni ya kizamani.
“Siwezi kupanga mahari, sijui laki nane au laki ngapi. Kiasi chochote ni sawa cha msingi mwanangu awe amekubaliana na huyo mwanaume.
“Hajaniambia kama kuna mtu anataka kuleta mahari,” alisema mama Lulu.
Kwa upande wake Lulu alisema: “Kwa sasa sina wazo la kuolewa ila naweza kuamka kesho nikabadili uamuzi.” Alipoulizwa kama ni kweli atatakiwa kulipiwa mahari ya laki nane alisita kidogo.
Kuhusu kigezo cha dini staa huyo alikiri kuwa kati ya vitu anavyozingatia ni hicho kwani hataki mwanaume wa kumbadilisha dini na mahari yake itategemea na mtoaji
KWA NINI LAKI 8?
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa wanandoa wengi waliofunga pingu za maisha hivi karibuni ulibaini kwamba wengi walilipa mahari ya kati ya shilingi laki sita na milioni moja na nusu huku wastani ukiwa ni shilingi laki nane