Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekabidhi shilingi Bilioni 12 kwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, zilizobaki
baada ya uchaguzi mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais uliofanyika tarehe
25 Oktoba, 2015.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damian Lubuva
amekabidhi hundi ya kiasi hicho cha fedha kwa Rais Magufuli leo tarehe
07 Juni, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa bakaa ya
fedha hizo haikuathiri kwa namna yoyote uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
"Mheshimiwa Rais fedha ambazo tunakukabidhi, tulijibanabana sana, japo
muda wenyewe ulikuwa mfupi lakini tulijibanabana sana bila kuathiri
utendaji wa shughuli za uchaguzi, isije ikawa inatoa sura kwamba
iliathiri, haikuathiri, na katika hali hiyo kama ambavyo wengi ni
mashahidi, hatujisifii, lakini uchaguzi ulienda vizuri" Amesema Jaji
Mstaafu Lubuva.
Akizungumza baada ya kupokea mfano wa hundi hiyo, Rais Dkt. John Pombe
Magufuli ameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuokoa fedha hizo na
kuzirejesha serikalini ili zipangiwe majukumu mengine na ametaka taasisi
nyingine za serikali ziige mfano huo wa uzalendo na kutanguliza maslahi
ya taifa.
"Kitendo hiki ambacho mmekionesha leo, kinaonesha ni kwa namna gani Tume
ya Taifa ya Uchaguzi chini ya uongozi wako Mheshimiwa Mwenyekiti ilivyo
na watu makini na waadilifu sana, kwa sababu hizi fedha ambazo kwa
lugha uliyotumia ni bakaa, kutokana na zile ambazo mlipewa zaidi ya
Shilingi Bilioni 270, mkatumia shilingi Bilioni 261.6, mkabakiza
shilingi Bilioni 12, mngeweza kuamua kusema hamkubakiza na hakuna mtu
yeyote ambaye angewauliza, na saa nyingine pengine hakuna mtu yeyote
ambaye angejua, mngeweza pia kusema kiasi mlichotupa hakijatosha,
tunaomba mtuongezee ama mngetengeneza maneno mazuri mazuri ya matumizi,
bado nina uhakika serikalini wasingejua" Amesema Rais Magufuli.
Pamoja na kukabidhi hundi ya bakaa ya shilingi Bilioni 12, Mwenyekiti wa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damian Lubuva amemuomba Rais
Magufuli aisaidie tume hiyo kupata jengo lake la ofisi kwa kuwa hivi
sasa tume inatumia majengo ya kupanga ambayo yanaigharimu tume hiyo
takribani shilingi Bilioni 1 na Milioni 400 kila mwaka kwa kulipia kodi
ya pango, usafiri na gharama nyingine za uendeshaji.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli amelikubali ombi hilo na kuamua kuwa fedha
ambazo Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeziokoa (Shilingi Bilioni 12) kutoka
kwenye Uchaguzi Mkuu wa Mwaka jana zitumike kujenga ofisi ya tume, na
amependekeza ofisi hiyo ijengwe mkoani Dodoma.
"Na mimi ningefurahi zaidi kama hilo jengo lingejengwa Dodoma, kwa
sababu Dodoma ndio makao makuu ya nchi hii, na hasa kwa sababu Dodoma ni
katikati ya Tanzania" Amesisitiza Rais Magufuli.
Rais Magufuli pia amelikubali pendekezo la tume hiyo la kuanzishwa kwa
mfuko wa tume ya uchaguzi ambao utakuwa unakusanya fedha kila mwaka kwa
ajili ya uchaguzi mkuu unaofuata, badala ya kuendelea na utaratibu wa
sasa wa kusubiri mwaka wa uchaguzi ndipo zitengwe fedha zote za
kugharamia uchaguzi huo.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
07 Juni, 2016
Home »
KITAIFA
,
SIASA
» Rais Magufuli Apokea Shilingi Bilioni 12 Ya Tume Ya Uchaguzi Zilizokuwa Zimebaki Baada ya Uchaguzi Mkuu
Rais Magufuli Apokea Shilingi Bilioni 12 Ya Tume Ya Uchaguzi Zilizokuwa Zimebaki Baada ya Uchaguzi Mkuu
Jika Anda menyukai Artikel di blog ini, Silahkan
klik disini untuk berlangganan gratis via email, dengan begitu Anda akan mendapat kiriman artikel setiap ada artikel yang terbit di Creating Website