Wakati
 Polisi ikimshikilia kwa saa mbili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe 
mkoani Mwanza, jeshi hilo limefuta kongamano la kujadili Bajeti ya 
Serikali lililoandaliwa na ACT Wazalendo jijini Dar es Salaam huku 
kiongozi wake, Zitto Kabwe akisakwa. 
Jeshi
 hilo lilizuia mkutano wa hadhara wa Chadema uliokuwa ufanyike wiki 
iliyopita mjini Kahama ambako lilitumia mabomu ya machozi kuwatawanya 
wanachama na wafuasi wa chama hicho, katika kile kilichoelezwa kulikuwa 
na dalili za uvunjifu wa amani. 
Jeshi hilo pia lilizuia msafara wa viongozi wa chama hicho kuingia katika ofisi zake za Shinyanga walipokuwa wakielekea Mwanza. 
Taarifa
 iliyotolewa jana na msemaji wa chama hicho, Tumaini Makene ilieleza 
kuwa mbali na Mbowe, jeshi hilo pia lilikuwa linawashikilia Mwenyekiti 
wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Patrobas Katambi na Katibu 
Mkuu wa Bavicha, Julius Mwita. 
Wengine
 ni Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka na viongozi wengine na wanachama 
wa chama hicho waliokuwa wanashikiliwa katika kituo cha Polisi Nyakato, 
jijini Mwanza. 
Makene
 alisema tangu asubuhi ya jana, Mbowe na viongozi wenzake walikuwa 
wakizunguka katika maeneo kadhaa ya jijini Mwanza kuwasalimia wananchi 
katika ‘vijiwe’ mbalimbali kabla hawajakamatwa. 
Alisema, “Hadi sasa (saa 11 jioni) hakuna maelezo ya kushikiliwa kwao.” 
Kamanda
 wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alithibitisha kukamatwa kwa 
viongozi hao na kubainisha kuwa waliachiwa bila kufunguliwa kesi yoyote.
“Walikutwa
 Igoma Sokoni wakizungumza na wananchi. Mikutano ya namna hii imezuiwa. 
Wamefungua kesi mahakamani, hivyo hakuna haja ya kufanya tofauti mpaka 
itakapohukumiwa,” alisema Msangi. 
Alifafanua kuwa jeshi hilo halina uhasama wowote na Chadema au chama kingine chochote na "hatuwezi kukiingilia kinapofanya mikutano yake ya ndani au hotelini. Kilichozuiwa ni mikutano ya hadhara.” 
Wakati
 Msangi akisema hayo, kongamano la ACT Wazalendo ambalo lilitakiwa 
lifanyike jana kuanzia saa 7:00 mchana kwenye Ukumbi wa Jengo la LAPF; 
Millennium Towers, Kijitonyama lilizuiwa na polisi. 
Tangu mapema asubuhi, askari polisi walitanda katika eneo la ukumbi huo kuzuia kongomano hilo. 
Ukumbini
 hapo, waandaaji walisema hakuna anayeruhusiwa kuingia kwani wamepewa 
maelezo ya kuufunga baada ya tukio lililoandaliwa kuahirishwa. 
Zaidi
 ya viti 210 vilikuwa vimepangwa kwa ajili ya kongamano hilo na mmoja wa
 viongozi wa ukumbi huo alionekana akiondoa mabango yaliyokuwa 
yanautambulisha mkutano huo wa ACT. 
Viongozi
 watatu wa ukumbi huo walikataa kueleza kinagaubaga juu ya sakata hilo, 
lakini taarifa za jumla zilisema mkutano umezuiwa. 
Mmoja wa watumishi wa ukumbi huo, alisema: “Tuliandaa kila kitu, ila shughuli imeahirishwa. Ukumbi unatakiwa kufungwa. Hautatumika kwa leo.” 
Ilipofika
 saa 5:00 asubuhi, Msemaji wa ACT-Wazalendo, Abdallah Khamis alisema 
chama kinafanya mkutano wa dharura kwenye ofisi zake za makao makuu na 
baadaye kingezungumza na waandishi wa habari. 
Saa
 8:00 mchana, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Anna Mghwira akiwa na 
viongozi wenzake, isipokuwa Kiongozi wa Chama, Zitto Kabwe alikuwa mbele
 ya kamera za wanahabari akifafanua kilichotokea kwa wanachama, wafuasi 
wa chama hicho na Watanzania kwa ujumla. 
Alisema
 ilipotimu saa 4:00 asubuhi walipewa taarifa na mwenye ukumbi kuwa Jeshi
 la Polisi Mkoa wa Kinondoni limemjulisha kuwa chama hicho hakina kibali
 cha kuendesha kongamano hilo na kwamba kisiruhusiwe kufanya hivyo. 
“Huku ni kufifisha demokrasia. Wapigania haki za kiraia wasimame imara na vyama vya upinzani katika kuilinda,” alisema Mghwira. 
Wakati
 kongamano hilo likizuiwa, kuna taarifa za kukanganya juu ya alipo Zitto
 baada ya kudaiwa alikuwa anasakwa na polisi tangu juzi. 
Taarifa
 hizo zinakuja siku chache baada ya kiongozi huyo kuitwa Kituo Kikuu cha
 Polisi jijini Dar es Salaam na kuhojiwa juu ya kauli alizozitoa kwenye 
mkutano wa hadhara zinazokosoa utendaji wa Serikali na kupinga matokeo 
ya uchaguzi wa Zanzibar. 
Baadaye jioni, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Msafiri Mtemelwa alitoa taarifa kuwa Zitto ametoweka na hajulikani alipo. Hiyo ilikuwa ni baada ya askari kanzu kumtafuta kwa muda kwa saa kadhaa. 
“Zitto
 amekuwa akitafutwa kwa muda mrefu. Askari wanalinda nyumbani kwake 
tangu jana (juzi) usiku. Hivi sasa ametoweka, hatujui alipo. Lolote 
litakalompata, Jeshi la Polisi litajibu,” alisema Mtemelwa. 
 

 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
