ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amelazwa tena katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu.
Jana, Ofisa Uhusiano Msaidizi wa MNH, Neema Mwangomo, alisema Kardinali Pengo alifikishwa hospitalini hapo jana saa nne asubuhi.
“Askofu aliletwa jana saa nne asubuhi na alilazwa katika kitengo chetu cha dharura ambapo madaktari walikuwa wakimfanyia uchunguzi wa afya yake,” alisema.
Siku chache zilizopita, Askofu Pengo alilazwa katika Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyoko hospitalini hapo kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.
Januari mosi, mwaka huu Rais Dk. John Magufuli pamoja na mkewe, Janeth walikwenda kumjulia hali askofu huyo.
Askofu Pengo aliruhusiwa kurudi nyumbani Januari 8 baada ya madaktari kuridhishwa na afya yake